Thursday, 29 May 2014

Rais Goodluck atangaza vita vikali


Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameagiza kufanywa oparesheni kali zaidi ili kudhibiti alichokiita mauaji ya kiholela yanayofanywa na magaidi.

Katika hotuba yake kwa taifa kuadhimisha siku ya demokrasia, rais Jonathan alitaja utekaji nyara wa zaidi ya wasichana mia mbili wa shule na kundi la Boko Harama kuwa unyama usiokubalika kamwe.
Waandishi wa habari hata hivyo wanasema kuwa haijulikani rais Jonathana anazungumzia kuchukua hatua zipi au ni oparesheni gani itafanywa kwa sababu tayari eneo hilo la Kaskazini mashariki mwa Nigeria tayari limewekwa chini ya hali ya hatari.

Rais Jonathan pia ameahidi kufanya mashauriano na upatanishi na watu watakaoweka silaha chini na kukoma kujihusisha na ugaidi.


Alipongeza jamii ya kimataifa kwa kuisaidia Nigeria kukabiliana na tatizo la ugaidi na usalama kwa jumla.
Rais Jonathan ameahidi kushughulikia swala la umasikini ambalo limechochea harakati kama za Boko Haram, lakini akasisitiza hilo litafanyika tu ikiwa ugaidi unaotendwa na Boko Haram utakapokomeshwa.

Benki ya dunia inasema kuwa zaidi ya watu milioni miamoja na kumi na tatu wanaishi kwa umaskini katika taifa hilo linalozalisha kiwango kikubwa zaidi cha mafuta Afrika.

Rais Goodluck, ametoa fursa kwa Boko Haram ikiwa wanataka kufanya mazungumzo na serikali kama njia ya kusuluhisha matatizo yao.

Maelfu ya watu wameuawa katika miaka mitano ya harakati za kundi hilo.Mwaka huu pekee watu 2,000 wameuawa huku zaidi ya wengine 750,000 wakiachwa bila makao.

CECAFA:Michuano yaingia robo fainali

Mashindano ya kandanda ya kombe la Cecafa Nile Basin yanaingia robo-fainali Ijumaa na Jumamosi nchini Sudan huku timu mbili za Sudan, Al Merreikh na Al Shandy, na AFC Leopards ya Kenya zikiongoza makundi yao.

Al Merreikh na Victoria ya Uganda zilimaliza mechi zao za makundi na pointi saba kila mmoja lakini Merreikh ikaongoza kundi A kwa sababu ya wingi wa mabao.
Merreikh sasa itakutana na Academie ya Tchite Burundi ambayo Jumatano ilimeza bao 1-0 dhidi ya AFC Leopards ya Kenya, mfungaji akiwa ni Bernard Mangoli.

Victoria inapepetana na Mbeya City, Leopards dhidi ya Defence ya Ethiopia, Al Shandy inakwaruzana na jirani wao wa Sudan Kusini, Malakia.

Katika mechi za Jumatano, Leopards ilishangiliwa sana na baadhi ya wanafunzi wa Kenya wanaosomea Sudan pamoja na balozi wa Kenya nchini humo Abrown Suge na naibu wake Maurice Nakitare.

Leopards itakua bila wachezaji wake mhimu Allan Wanga, Jacob Keli, James Situma na Wycliffe Kasaya ambao wako na timu ya taifa Harambee Stars kwa mechi yao na Comoros Ijumaa ya kufuzu kwa fainali ya mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika.

Etincelles imerudi nyumbani bila ushindi, na hawatasahu mechi yao ya mwisho dhidi ya Mbeya City waliposhindwa kufunga penalti, huku Al Shandy ikiicharaza Defence mabao 2-0, wafungaji wakiwa ni Nadir Eltyab na Omar Mahmoud.

Ghasia zaidi kupinga kombe la dunia

Polisi nchini Brazil wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji katika mji mkuu Brasilia wanaopinga kuandaliwa kwa kombe la dunia nchini humo.

Polisi walipigwa kwa mawe huku mamia ya waandamanaji wakijaribu kufika uwanja wa kitaifa ambako kombe litakalopokezwa washindi wa kinyang'anyiro hicho limewekwa.

Kikundi cha watu asilia wanaodai haki zao za kumiliki ardhi walijiunga na maandamano hayo.
Haya ni maandamano ya hivi karibuni nchini Brazil kupinga gharama iliyotumiwa kuandaa kombe hilo.

Maafisa wakuu wanasema kuwa karibu watu 1,500 walihudhuria maandamano hayo yaliyofanyika Jumanne.
Waandamanaji hao walijaribu kwenda katika uwanja wa kitaifa ambao utakuwa mwenyeji wa mechi kadhaa za kombe la dunia ingawa polisi waliwazuia.

Polisi mmoja alijeruhiwa kwa mshale uliorushwa na mmoja wa waandamanaji wakati wa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji hao.

Waandamanaji hao walitatiza pakubwa msongamano wa magari mjini Brasilia kwa masaa kadhaa.
Mwaka jana takriban watu milioni moja walishiriki maandamano kote nchini humo kutaka huduma bora zaidi za umma na kulalamikia ufisadi na gharama ya juu iliyotumiwa kuandaa kombe la dunia.

Manchester United mayatima

Mmiliki wa Manchester United mmarekani Malcom Glazer ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 85 .
Familia ya bwenyenye huyo ilinunua United kwa gharama ya Euro milioni 790 mnamo mwezi Mei mwaka wa 2005 licha ya pingamizi kali kutoka a kwa mashabiki wa klabu hiyo.
Hata hivyo, Chini ya umiliki wake uliosabibisha deni kubwa kwa klabu hiyo ''the Red Devils'' walishinda taji la premia ya Uingereza mara tano na vile vile taji la klabu bingwa mwaka wa 2008 .

Wanawe mmarekani huyo waliozaliwa Marekani Byan, Joel, na Avram wote wamejumuishwa katika bodi ya klabu hiyo, huku Joel na Avram wakiwa wenyekiti wenza.

Kifo cha Glazer hakitarajiwi kuadhiri umiliki wa United, kwani familia hiyo bado inamiliki asilimia 90 za hisa za klabu hiyo .

Asilimia 10 inayosalia inamilikiwa na wenyehisa katika soko la hisa la NY stock Exchange.

Mmiliki wa Man united ameaga dunia ambapo pia alikuwa pia mmiliki wa Tampa Bay Buccaneers, iliyobadili sura ya kandanda ya Marekani kwa kushinda taji la Super Bowl .
Bwenyenye huyo ambaye hakuwahi kukanyaga uwanjani Old Trafford kutokana na hofu ya kuwaudhi mashabiki wa timu hiyo ambao walikuwa wanamsuta kwa kupanga njama ya kuinunua klabu hiyo kwa kutumia madeni.

United ambayo msimu uliopita ilitangaza faida kubwa ya asilimia 20 yaani pauni milioni 418 inakabiliwa na deni la zaidi ya pauni milioni 400.

Glazer aliyeugua kiharusi tangu mwaka wa 2006 amewaachia wanawe sita umiliki wa klabu hiyo ya Uingereza.

BILAL ATEMBELEA KIWANDA CHA KUKAMUA MAFUTA YA UFUTA CHA TAKEMOTO, NAGOYA JAPAN





Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib 
Bilal, mkewe Mama Asha Bilal, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Salome Sijaona 
(wa pili kushoto) na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaki Okada, wakiongozana 
wakati walipokuwa wakielekea kutembelea kiwanda cha kukamua mafuta ya Ufuta cha Takemoto kilichopo Nagoya nje kidogo ya Jiji la Tokyo Japan, jana Mei 22, 2014, 
akiwa katika ziara yake ya kikazi nchini Japan. Picha na OMR

Monday, 26 May 2014

WAKUDATA: YAPANDA CHATI KWA KUCHEKESHA

Katuni maarufu ya  wakudata inazidi kupanda chati baada ya idadi kubwa ya watu kuomba kukutana na mchoraji wa katuni hizo Said Michael, ambazo zinaongoza kwa kutoa vionjo vya kuchekesha na kuburudisha kila siku kupitia gazeti la Tanzania Daima.

Msama ampongeza Mwakyembe kuifufua ATCL




Na Mwandishi wangu

SERIKALI kupitia Wizara ya Uchukuzi inayoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe inastahili, pongezi kwa kupiga hatua kubwa kujenga na kuimarisha sekta ya usafirishaji wa anga nchini.

Mkurugenzi wa Msama Promotins Alex Msama, ametoa pongezi hizo siku chache baada ya Wizara hiyo kuendelea kuonesha mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za anga nchini.

Msama ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu amewahimiza Watanzania kujawa na uzalendo na hivyo, kuliunga mkono Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kutumia huduma zake zilizoboreshwa ili liweze kupambana na changamoto  mbalimbali zilizopo katika sekta ya usafirishaji wa anga nchini.

Alisema hatua ya Wizara ya Uchukuzi kuwekeza katika usafiri wa anga inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania kwa maslahi ya taifa.

“Huduma zinazotolewa na ATCL sasa ni nzuri na zenye ubora unaolingana na mazingira ya sasa, hivyo ni vema sisi Watanzania tujivunie; kila Mtanzania anapaswa kujivunia na kutumia huduma za shirika hilo.” 

Hata hivyo, alitoa rai kwa makampuni, taasisi zote za serikali na mtu mmoja mmoja kutumia ndege ya shirika hilo linalofanya safari zake katika mikoa mbalimbali nchini. Kwamba hatua pekee ya kuongeza ufanisi wa ATCL ni watu kutumia  chao na kukilinda na kukituza.

Mpaka sasa ATCL ina ndege mbili ikiwamo ya Jet 103, ambazo kwa muda mfupi, zimeonesha ufanisi wa hali ya juu katika utoaji huduma wa safari za anga.

Aliongeza kuwa amefurahishwa na huduma ya Ndege ya ATCL itokayo Dar kwenda Mwanza ambapo alisema kuwa ndege hiyo ni nzuri na pia huduma zake ni nzuri na ikiwa angani inatulia mpaka unajisahau kama upo ndani ya ndege.

Aidha alisema kuwa ni vyema kila mtanzania akatumia ndege hii kwani kwa ndege zote alizopanda kwenda Mwanza hii ni ndege bora zaidi.

Pia amewaasa Watanzania kuwa wazalendo kama wenzetu wakenya ambao wamekuwa wazelendo kwa kutumia ndege zao kila wafanyapo safari, na hivyo ni vema watanzania  kutumia ndege za ATCL ili kusaidia shirika hilo kutoka ndege mbili hadi kuongeza ndege zaidi.

VIONGOZI WA 'PANYA ROAD' MBARONI


Kamishna wa Kanda Maalum ya Mkoa Dar es salaam Suleiman Kova akiwaonesha waandishi wa habari picha ya viongozi 7 wa kundi la uharifu maarufu kama “Panya road” waliokamatwa jijini Dar es salaam juzi katika msako uliofanyka maeneo ya kigogo.

Sunday, 18 May 2014

BLATTER : AIKOSOA QUATAR

Mwenyekiti wa shirikisho la kandanda ulimwenguni, FIFA, Sepp Blatter, amesisitiza ilikuwa kosa kuchagua Quatar kuwa mwenyeji wa kombe la dunia la mwaka wa 2022.

Katika mahojiano na televisheni nchini Uswizi, Sepp Blatter aliulizwa iwapo kuiruhusu Quatar kuwa mwenyeji wa kombe hilo ambalo huchezwa kati ya mwezi Juni na Julai ilikuwa kosa, hasa ikizingatiwa kuwa hali ya hewa katika nchi hiyo hufikia hadi nyuzijoto 50 wakati huo.

Alijibu kwa kukiri na kuongeza kuwa kila mtu hukosea maishani. Alipinga madai kwamba taifa hilo lilikuwa limelipia michezo hiyo.

Aliongeza kuwa kamati inayojumuisha maafisa wa FIFA walikuwa wamedhibitisha uwezekano wa taifa hilo kuwa mwenyeji ijapokuwa walikuwa wamepokea taarifa kuhusu vipimo vya juu vya joto.


Alisema kwamba michezo hiyo badala yake inaweza kusogezwa hadi miezi ya mwisho wa mwaka, wakati vipimo vya joto vitakuwa vimepungua.

SADIK: USAFI KWA WOTE


3     Mkuu wa mkoa wa Dar esSalaam Said Meck Sadik (wa kwanza kulia), akifuatiwa na Meya wa Manispaa ya Kinondoni Yusuph Mwenda, wakiwaongoza wananchi wa manispaa ya Kinondoni kufanya usafi katika mto mlalakuwa kwa ajili ya kupambana na maradhi yanayozalishwa uchafu

SIMBA MAMBO MOTO

Katibu Mkuu Msaidizi wa Kamati ya Uchaguzi wa klabu ya Simba, Kamguna Aman akimkabidhi fomu mgombea wa Urais wa klabu hiyo, Michael Wambura katika Makao Makuu ya klabu hiyo jana


Thursday, 15 May 2014

YOUNG KILLER, FID Q WAPOKEWA KIFALME MWANZA


Na Mika Ndaba
WASANII wa muziki wa hip hop wanaouwakilisha mkoa Mwanza, Farid Kubanda ‘Fid Q’ na Erick Msodoki ‘Young Killer’ wanatarajiwa kupokelewa kifalme katika mkoa huo baada ya kuchukua tuzo za Kilimanjaro Music Awards.

Katika tuzo hizo zilizotolewa Mei 3 ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Mkongwe wa muziki wa hip hop, Fid Q alichukua tuzo mbili za mtunzi bora wa mashairi ya hip hop na msanii bora wa hip hop huku Young Killer akipata tuzo ya msanii bora anayechipukia. 

Akizungumza Indaba Blog
 jijini Dar es Salaam juzi, Young Killer, alisema, kuna mdau ambaye yupo jijini Mwanza ndio anawaandalia sherehe hiyo hivyo anaomba wadau wa mkoa huo wakae mkao wa kula.


“Binafsi sijapewa taarifa rasmi kama ni lini itafanyika, Mwanza ni mkoa ambao unakubali wasanii wake mimi nitashukuru ikiwa hivyo, naomba mashabiki wajiandae kupata burudani iliyokamilika,” alisema.

Mbali na hilo, Young Killer alitambulisha video ya ngoma yake inayojulikana kwa jina la ‘Masaa’ ambayo inafanya vizuri katika vituo mbalimbali vya redio.

“Hii ni video yangu mpya naomba mashabiki waipokee najua wapenzi wangu wananijua sifanyi vitu kwa kubahatisha hii ni bonge la video naweza nikasema ni video ya mwaka kwasababu inaviwango vya hali ya juu, kikubwa ni sapoti kutoka kwa wadau,” alisema.

Kwa upande wake Fid Q, alisema anawashukuru Watanzania na waandaaji wa tuzo hizo, kwa kutambua mchango wake katika tasnia ya muziki hivyo anaahidi kufanya mambo mazuri ili aendelee kuwa bora katika fani hiyo.

“Sitaki kupoteza sifa yangu niliyoipata mwaka huu nataka iendelee miaka yote, nawahaidi mashabiki wangu nitaendelea kufanya kazi nzuri ambazo zitawavutia siku zote,” alisema.