Thursday, 15 May 2014

YOUNG KILLER, FID Q WAPOKEWA KIFALME MWANZA


Na Mika Ndaba
WASANII wa muziki wa hip hop wanaouwakilisha mkoa Mwanza, Farid Kubanda ‘Fid Q’ na Erick Msodoki ‘Young Killer’ wanatarajiwa kupokelewa kifalme katika mkoa huo baada ya kuchukua tuzo za Kilimanjaro Music Awards.

Katika tuzo hizo zilizotolewa Mei 3 ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Mkongwe wa muziki wa hip hop, Fid Q alichukua tuzo mbili za mtunzi bora wa mashairi ya hip hop na msanii bora wa hip hop huku Young Killer akipata tuzo ya msanii bora anayechipukia. 

Akizungumza Indaba Blog
 jijini Dar es Salaam juzi, Young Killer, alisema, kuna mdau ambaye yupo jijini Mwanza ndio anawaandalia sherehe hiyo hivyo anaomba wadau wa mkoa huo wakae mkao wa kula.


“Binafsi sijapewa taarifa rasmi kama ni lini itafanyika, Mwanza ni mkoa ambao unakubali wasanii wake mimi nitashukuru ikiwa hivyo, naomba mashabiki wajiandae kupata burudani iliyokamilika,” alisema.

Mbali na hilo, Young Killer alitambulisha video ya ngoma yake inayojulikana kwa jina la ‘Masaa’ ambayo inafanya vizuri katika vituo mbalimbali vya redio.

“Hii ni video yangu mpya naomba mashabiki waipokee najua wapenzi wangu wananijua sifanyi vitu kwa kubahatisha hii ni bonge la video naweza nikasema ni video ya mwaka kwasababu inaviwango vya hali ya juu, kikubwa ni sapoti kutoka kwa wadau,” alisema.

Kwa upande wake Fid Q, alisema anawashukuru Watanzania na waandaaji wa tuzo hizo, kwa kutambua mchango wake katika tasnia ya muziki hivyo anaahidi kufanya mambo mazuri ili aendelee kuwa bora katika fani hiyo.

“Sitaki kupoteza sifa yangu niliyoipata mwaka huu nataka iendelee miaka yote, nawahaidi mashabiki wangu nitaendelea kufanya kazi nzuri ambazo zitawavutia siku zote,” alisema.

No comments:

Post a Comment