Friday, 25 July 2014

WANAFUNZI WATAKIWA KUPENDA MASOMO YA SAYANSI



NA MAGIGI JOHN


WANAFUNZI wa shule mbalimbali nchini wametakiwa kujifunza  masomo ya sayansi kutokana na umuhimu wake katika ugunduzi wa vitu ili kusaidia taifa kimaendeleo.


Imeelezwa kuwa idadi kubwa ya wanafunzi na walimu ukimbia masomo hayo, kiasi cha kusababisha watu kuamini masomo hayo ni magumu hasa kwa jinsi yanavyofundishwana.


Akitoa rai hiyo jijini Dar es Salam jana, Mkurugenzi wa Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi (YS), Dr. Gozibert Kamugisha alieleza kuwa taifa linakabiliwa na changamoto ya wataalamu wa masomo hayo, hivyo kusababisha taifa kutofikia hatua ya kugundua vitu kama ilivyo kwa nchi nyingine.


Kamugisha alisema kuwa, idadi kubwa ya wanafunzi na walimu wanashindwa kujua jinsi ya kujifunza masomo hayo hatimaye kuchangia ongezeko kubwa la upungufu wa wasomi kwenye sekta ya Sayansi.


“Wanafunzi wengi wanajifunza sayansi kwa njia ya kukalili na sio vitendo, hivyo kuna tija tubadilike ili nchi yetu iendane na mifumo mipya inayoendana na mabdiliko ya dunia hasa kwa vitendo” alisema Kamugisha.


Alisema kuwa, miongoni mwa masomo ambayo yanakimbiwa ni Hesabu, Fizikia, Biolojia, Kemia na somo la Sayansi ya Jamii, hivyo kupunguza idadi ya ugunduzi wa vitu mbalimbali vinavyofanywa na watu wengine duniani.

No comments:

Post a Comment