Monday, 5 May 2014

WAZAZI  nchini  wametakiwa  kuwashawishi wanafunzi wa kike kupenda  masomo ya sayansi,  ili kukabiliana na wimbi la upungufu wa wakunga.

Akizugumza hayo jijini Dar es Salaam  jana katika Sherehe za Maazimisho ya Siku ya Wakunga duniani Mke wa Rais,  Mama Salma Kikwete alisema kuwa,  wazazi na jamii  wanatakiwa kutambua  sekta ya Afya inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wakunga  kwakuwa watoto wengi wa kike wanakimbia masomo ya sayansi.

Alisema kuwa, kuna haja ya kupigania watoto wa kike wapate elimu ya kutosha juu ya masomo ya sayansi ili kuongeza idadi ya wakunga, ambao watasambaa katika nchi nzima ili kupunguza idadi ya vifo vya mama wajawazito na watoto.

“Kuna changamoto nyingi sana ambazo zinaathiri utoaji huduma, kwa kufuata miongozo na viwango vilivyo wekwa .Hivyo basi napenda kuchukua nafasi hii kuwaasa wakunga wote  kwa kazi  wanazofanya kwani ni muhimu.” alisema  mama Salma.

Kwa upande Rais wa  Chama cha wakunga Tanzania,   Feddy Mwanga alisema  kuwa,  idadi kubwa ya wanawake wanajifungulia majumbani na hivyo kuhatarisha afya zao kwakuwa bado hawajapewa elimu ya kutosha kuhusu uzazi salama.

“Katika hali halisi iliyopo ya upungufu mkubwa wa wakunga, vituo vya kutolea huduma na vifaa duni vya kufanyia kazi imekuwa sababu kubwa ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto hapa Tanzania .Mkunga mmoja analazimika kuhudumia wajawazito zaidi ya 40 .Hivyo  kuna uhitaji mkubwa sana wa wakunga  hapa ncini” alisema Mwanga.


No comments:

Post a Comment